Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimeibuka na kuutaka uongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), umfukuze uanachama aliyekuwa mgombea urais kupitia chama hicho, Edward Lowassa.
Hatua hiyo ya CCM imekuja siku moja baada ya Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, kusema ufisadi ni ajenda yao ya kudumu. Kutokana na kauli hiyo ya Lissu, CCM imetaka Chadema imfukuze Lowassa, ili kutekeleza kwa vitendo kauli ya Lissu .
Lowassa ambaye ni Waziri Mkuu mstaafu, alihama CCM baada ya kuenguliwa kuwania urais kupitia chama hicho na kujiunga na Chadema ambako alipewa nafasi ya kugombea urais kupitia chama hicho na kuungwa mkono na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Aidha, CCM imeitaka Chadema kutangaza hadharani kumuunga mkono Rais Dk. John Magufuli, kwa kazi anazozifanya, ikiwamo kukemea ufisadi badala ya kuzungumza kwa maneno bila vitendo.
Kauli hiyo, ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Katibu wa Nec, Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnaye, ambaye alisema chama hicho kimekosa ajenda kwa kuwakumbatia mafisadi.
“Tundu Lissu nimemwelewa alichokisema lakini waache kuwahadaa Watanzania kuwa ufisadi ni ajenda yao. Wakitaka kufanya hivyo kwanza wamfukuze Lowassa na pia watangaze hadharani kumuunga mkono Rais Magufuli. Hapo tutawaelewa badala ya kuzungumza tu bila vitendo,” alisema Nape.
Akizungumzia sababu za CCM kutomfukuza Lowassa akiwa ndani ya chama hicho, alisema jambo hilo lilifanyika kupitia kampeni yake ya vua gamba.
“Tulianzisha kulishughulikia suala la ufisadi ndani ya chama tangu enzi za kuvua gamba na kama unavyoona hatimaye aliondoka. Lakini ifahamike kuwa kila jambo linafanyika kwa wakati wake,” alisema.
Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki, jana alinukuliwa na gazeti moja (si Nipashe) akisema kuwa chama chake kitaendeleza ajenda ya mapambano dhidi ya ufisadi kwa kuwa ajenda za taifa ni nyingi na Rais Magufuli hataweza kuzitekeleza.
Katika hatua nyingine, CCM imesema inatarajia kuadhimisha miaka 39 ya kuzaliwa kwake ambayo kitaifa yatafanyika mkoani Singida Februari 6, mwaka huu.
Nape alisema uzinduzi wa maadhimisho hayo, utafanyika Januari 31 kisiwani Unguja na kwamba mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein.
Alisema maadhimisho hayo yenye kaulimbiu ‘Sasa Kazi, Kujenga Nchi na Kukijenga Chama’, yatatanguliwa na shughuli za mbalimbali za maendeleo katika mikoa yote nchini.
Alizitaja shughuli hizo kuwa ni kuingiza wanachama wapya na kufanya mikutano ya kuwashukuru wananchi kwa kukichagua tena chama katika ngazi ya urais, wabunge na madiwani.
Kwa mujibu wa Nape, kilele cha siku ya kuzaliwa kwa CCM huadhimishwa Februari 5 kila mwaka, lakini mwaka huu kitakuwa Februari 6 kwa sababu Februari 5 itakuwa siku ya kazi.
By Lios media