Friday, 3 January 2020

Mwandishi wa habari Erick Kabendera anyimwa ruhusa ya kumzika mama yake

LIOS MEDIA ,
Dar es salaam Tanzania
03/01/2020


Mwandishi wa habari Erick Kabendera aliyeko rumande anyimwa ruhusa ya kwenda kumuaga au kumzika mama yake.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam imemnyima mwandishi wa habari Erick Kabendera aliye rumande ruhusa ya kwenda kumuaga au kumzika mama yake.
Mama yake Kabendera, Bi Verdiana Mujwahuzi, alifariki dunia siku ya Jumanne tarehe 31 Desemba 2019 katika hospitali ya Amana jijini Dar es Salaam.
Akitoa uamuzi wa mahakama hiyo, Hakimu Mkazi Mkuu, Janeth Mtega alisema mahakama hiyo haina mamlaka ya kutoa amri ya Kabendera kusindikizwa chini ya ulinzi kwenda kutoa heshima za mwisho kwa marehemu mama yake mzazi.
Uamuzi huo ulikuja katika awamu ya pili ya usikilizwaji wa kesi hiyo baada ya upande wa mashitaka na utetezi, kubishana kwa hoja kwa saa kadhaa na baadae hakimu kuahirisha usikilizaji hadi baadae ambapo hakimu alikuwa tayari kutoa uamuzi wa mahakama.
Awali, upande wa utetezi ulitoa hoja kadhaa za kwanini mahakama itoe amri kwa Kabendera kuruhusiwa kwenda kumuaga ama kumzika marehemu Mama yake mzazi.
Mmoja wa mawakili wa Kabendera Jebra Kambole aliiambia mahakama kuwa, suala la mtu kuhudhuria sala ya mwisho ya msiba ni haki ya msingi ya binadamu, ni haki ya faragha ya kuwa na familia kama ilivyoainishwa katika Ibara ya 16 katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977.
Mwandishi Erick Kabendera akiwa na wakili wake Jebra Kambole
Lakini aliongeza pia kwamba haki hiyo inaambatana na kutimiza dhana kwamba mtuhumiwa hana hatia hadi pale itakapothibitishwa na mahakama kama ilivyoelezwa na katiba pia.
"Kwa kumzuia kuhudhuria heshima ya mwisho ya mama yake tutakuwa tunamuadhibu na adhabu hiyo itakuwa ni kubwa sana na ya kinyama kushindwa kuhudhuria maziko ya mama yake" aliongeza wakili Kambole.
Wakili Kambole aliongeza kwamba wakati mahakama inafanya maamuzi juu ya ruhusa hiyo ni muhimu yazingatie uhusiano uliokuwepo kati ya marehemu na mfiwa, mama na mtoto.
Aliikumbusha mahakama kwamba Kabendera ndiye ambaye alikuwa akimuuguza mama yake kabla ya kukamatwa kwake na kwamba ni vyema basi akaruhusiwa angalau kwenda kutoa heshima za mwisho kwa marehemu mama yake.
Hata hivyo upande wa mashtaka ulisimama na kupinga hoja hizo na kudai kwamba mahakama hiyo ya hakimu mkazi haina mamlaka ya kisheriaya kutoa amri ya kupelekwa Kabendera kwenda kumuaga mama yake.
"Maombi yameletwa si kwa wakati sahihi kwamba mahakama haina mamlaka Hata kama sisi tunasikitika kwamba ni msiba mkubwa lakini taratibu za kisheria ni muhimu kuzingatiwa" alisema Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon.
Wakili Simon alidai kwamba hii si mara ya kwanza kwa mahabusu kufiwa, lakini pia hoja za upande wa utetezi hazina nguvu ya kisheria.
Kufuatia uamuzi huo wa mahakama, upande wa utetezi umesema hata kama wanakubaliana na dhana ya mahakama ya hakimu mkazi kutokuwa na mamlaka ya kisheria katika kesi ya kiuchumi kama hii, haukubaliani na uamuzi wa mahakama kumnyima Kabendera fursa ya kumuaga Mama yake kwa mara ya mwisho
Kuhusu mchakato wa 'plea bargain', upande wa mashtaka ulisema upande wa utetezi umekamilisha marekebisho katika maombi yao waliyotakiwa kufanya, hivyo mchakato huo unaendelea
Kesi ya Kabendera imeahirishwa zaidi ya mara kumi, na leo pia imeahirishwa na kupangiwa kusikilizwa tena tarehe 13 January 2020.

No comments:

Post a Comment

yes by message

HABARI

Fahamu matukio matano mabaya zaidi viwanjani yaliyoua mamia ya watu

  CHANZO CHA PICHA, GETTY IMAGES Raia wa Indonesia wanataka majibu ya moja ya maafa mabaya zaidi katika historia ya mchezo huo duniani, baad...