Mamlaka ya mawasiliano nchini Kenya imechapisha mwongozo mpya wa vipindi vya radio na televisheni.
Mwongozo
huo unanuia kudhibiti nyakati za kupeperusha matangazo na vipindi
vinavyolenga watu wazima na pia kuepusha matumizi ya lugha chafu na
gumzo za ngono.Mwongozo huo utakapotekelezwa pia utapiga marufuku kupeperushwa kwa vipindi vya kidini vyenye ujumbe wa kuomba pesa kwa waumini ili wapate baraka.
Mwaka uliopita, mhubiri mmoja aligonga vichwa vya habari baada ya makala ya ufichuzi kuonyesha akifanya miujiza bandia na kuwaomba watu wamtumie takriban $3 (£2) kupitia simu akisema ni baraka ndipo wapate baraka.
"Wahubiri hawafai kutumia dini kufaidi kutoka kwa watazamaji au wasikilizaji kwa kuwaomba wawasaidie kifedha au kushambulia imani ya mtu kwa kumshawishi mtu kubadili imani yake," mwongozo huo unasema.
Vipindi vya redio vinavyozungumzia ngono au masuala ya watu wazima, au kutumia lugha chafu pamoja na video zenye picha za uchi vyote havifai kupeperushwa kati ya saa kumi na moja asubuhi na saa nne usiku.
Hii ni mara ya kwanza hatua kama hiyo kuchukuliwa.
Kaimu mkurugenzi wa masuala ya wateja katika Mamlaka ya Mawasiliano ya Kenya Bw Christopher Wambua anasema mwongozo huo umeandaliwa baada ya majadiliano kati ya wadau mbalimbali mwaka jana.
"Mamlaka ilianza kutoa leseni za TV kwa mashirika mbalimbali baada ya kumalizika kwa kesi mahakamani ambayo ilikuwa imewasilishwa kupinga mamlaka ya mamlaka hiyo katika kudhibiti utangazaji. Mwongozo huu ni sehemu ya masharti ambayo watangazaji wanafaa kutii," Bw Wambua ameambia BBC.
"Mamlaka imewapa watangazaji miezi sita ya kutekeleza mwongozo huu. Muda huu utamalizika katikati mwa mwaka huu."
No comments:
Post a Comment
yes by message