Milipuko ya mabomu imetokea katika jiji kuu la Indonesia, Jakarta na baadaye ufyatulianaji mkali wa risasi na watu sita wanahofiwa kufariki.
Polisi wanasema washambuliaji wanne wamefariki.
Milipuko imetokea maeneo kadha, ikiwa ni pamoja na mgahawani katika duka la kibiashara lililoko karibu na ikulu ya rais na afisi za UN.
Kuna ripoti za maafisa wa polisi kuonekana kwenye majengo na barabara za mji huo karibu na kituo hicho cha kibiashara.
Eneo hilo limezingirwa na maafisa wa usalama.
Rais Joko Widodo amehimiza raia wawe na utulivu na kushutumu "kitendo hicho cha ugaidi".
"Tunaomboleza watu waliofariki kwa sababu ya kisa hiki, lakini pia tunakilaani. Kimevuruga utulivu na amani na kuingiza wasiwasi miongoni mwa raia," amesema.
Msemaji wa polisi Anton Charliyan ameambia wanahabari kuwa maafisa wa polisi na raia ni miongoni mwa waliofariki.
Bado haijabainika ni nani huenda amehusika katika shambulio hilo.
Indonesia, taifa lenye Waislamu wengi zaidi duniani, imeshambuliwa na makundi ya wapiganaji wa Kiislamu awali.
Majuzi, imekuwa kwenye hali ya juu ya tahadhari kutokana na tishio kutoka kwa wapiganaji wa Islamic State.
Hili ndilo shambulio la kwanza kubwa kutokea Jakarta tangu mashambulio kwenye hoteli za Marriot na Ritz mwaka 2009.
By Lios Media
No comments:
Post a Comment
yes by message