Saturday, 9 January 2016

OFISI ya Makamu wa Rais imesema msimamo wake wa kulibomoa hekalu la Mchungaji Geutrude Rwakatare, lililoko mtaa wa Ali Sykes, Kawe Beach uko pale pale kwa sababu limejengwa kinyume na taratibu za hifadhi ya mazingira.
 
Kauli hiyo ilitolewa jana kupitia taarifa kwa vyombo vya habari iliyokuwa ikizungumzia tathmini ya uvunjaji wa nyumba mbalimbali jijini Dar es Salaam.
 
Aidha, taarif hiyo ilibainisha siri ya ushindi wa Rwakatare mahakamani, ambako alipewa kibali cha kutobugudhiwa.
 
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, juzi ulifanyika mkutano wa mawaziri wanne wa Wizara mbalimbali ambao walipokea ripoti ya timu ya wataalam wa Wizara mbalimbali, inayoongozwa na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).
 
Mawaziri watatu waliokutana ni pamoja na (Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tamisemi na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais pamoja na Naibu Waziri wa  Maliasili na Utalii.
 
Mawaziri hao walifanya mkutano wa kutathmini zoezi la kuhamisha wakazi wa mabondeni katika Jiji la Dar es Salaam.  
 
Ilisema mkutano huo ulipokea taarifa kuhusu suala linaloongelewa sana la nyumba ya Mchungaji Rwakatare na kuelezwa kuwa amejenga nyumba yake mahali ambapo amezuia mtiririko wa mto kwa kujaza kifusi ili kupata eneo zaidi katika eneo la miti ya mikoko, kinyume kabisa na Sheria tatu muhimu.
 
Pia ilielezwa kwamba tangu wakati ujenzi unaanza jitihada za kumsimamisha zilifanyika na mamlaka za Serikali za Mitaa lakini ikashindikana kutokana na sababu mbalimbali na pale NEMC lilipoingilia kati na kutaka kuibomoa nyumba hiyo, Baraza lilishtakiwa mahakamani.
 
Taarifa hiyo ilisema wakati kesi inataka kuanza kusikilizwa, mwanasheria mdogo wa Baraza, yeye mwenyewe bila kuagizwa wala kuwaarifu wakubwa zake, Mei 11, 2015 aliingia makubaliano na mawakili wa Mchungaji Rwakatare kwa niaba ya Baraza ya kuondoa kesi hiyo mahakamani na kukubali, kwa niaba ya Baraza, na kutombughudhi kabisa Mchungaji Rwakatare.
 
Ilisema makubaliano hayo yalisajiliwa na Mahakama kama hukumu Mei 13, 2015 na Mwanasheria huyo wa NEMC alificha makubaliano hayo kwa miezi mitano hadi Oktoba 2015, yalipogundulika na mtumishi mwingine wa Baraza hilo.
 
Ilisema mkutano ulielezwa kwamba Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, kwa kufuata taratibu zote, alishaagiza kufukuzwa kazi, kukamatwa na kufunguliwa mashtaka kwa mwanasheria huyo na alifukuzwa kazi Januari 6, 2016 na taarifa zake zimekwishafikishwa Takukuru.
 
Aidha, Ofisi ya Makamu wa Rais, iliiagiza NEMC kufungua shauri mahakamani la kuomba “makubaliano” kati yake na Mchungaji Rwakatare yawekwe pembeni kwasababu yalipatikana na njia ya udanganyifu na shauri hilo lilifunguliwa Disemba 29, taarifa hiyo ilisema. 
 
Ilisema nyumba ya Mchungaji Rwakatare lazima itaondolewa kwa kuwa serikali ilishabaini udanganyifu uliofanywa na mtumishi wa NEMC aliyefukuzwa kazi hivi karibuni na kwamba alishirikiana na mawakili wa Mchungaji huyo kughushi nyaraka za serikali na kuficha ushahidi kwamba nyumba hiyo iko kwenye eneo la hifadhi ya mikoko.
 
Wakati huo huo, juzi NEMC ilitupilia mbali utetezi uliotolewa na Mchunguji wa Kanisa la Assemblies of God, Dk. Getrude Rwakatare, kuhusu alama ya X iliyowekwa kwenye jumba lake la kifahari na imepamga kuliangusha jumba hilo wakati wowote kuanzia sasa.
 
Desemba 31 mwaka jana, nyumba ya Mchungaji  Rwakatare iliyopo Kawe Beach, jijini Dar es Salaam  iliwekwa alama ya X  na maofisa wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), ambao walimtaka alibomoe mwenyewe kabla ya tinga tinga lao halijafika.
 
Baada ya kupita siku mbili tangu kuwekewa alama ya X, Mchungaji Rwakatare aliibuka na kusema kuwa nyumba yake iko eneo hilo kihalali na imefuata masharti ya (NEMC) na kwamba jengo hilo liko umbali wa mita 60 kama Sheria ya Baraza hilo inavyotaka.
 
Kwa mujibu wa Ofisa Misitu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Ismail Aluu, Mchungaji Rwakatare alipewa notisi hadi Alhamisi wiki hii awe amebomoa vinginevyo serikali itambomolea muda wowote itakaoona inafaa kufanya hivyo.
 
“Tunasubiri tuone kama muda tuliompa utapita bila yeye kutekeleza agizo letu kisha sisi tutakwenda na matinga tinga yetu kuliangusha,” alisema na kuongeza kuwa ingawa Mchungaji huyo alikwenda kwenye Mahakama ya Ardhi kwa ajili ya zuio wao bado hawajalipata hivyo wataendelea na utaratibu wao.
 
Aidha, alisema sababu ambazo Mchungaji Rwakatare alizitoa hivi karibuni hazina msingi wowote na ni kutapa tapa kwani kwa vipimo walivyofanya wamejiridhisha kuwa nyumba hiyo imejengwa kwenye uhifadhi wa mikoko kinyume cha Sheria.
 
Ofisa huyo alisema mwaka 2012 Rwakatare alijaza vifusi katika eneo hilo na walipomjulisha kuwa hatakiwi kufanya shughuli za ujenzi alikimbilia mahakamani huku shughuli za ujenzi zikiendelea.
 
Aidha, alisema kama kweli Mchungaji Rwakatare ana hati zinazoonyesha kuwa nyumba hiyo imejengwa kihalali maeneo hayo awaonyeshe ili wamchukulie hatua mtumishi wa serikali aliyempatia kibali hicho.
 
“Atuonyeshe hiyo hati inayompa uhalali wa nyumba yake kuwa pale ili tuwaulize Wizara ya Ardhi iweje wanatoa kibali cha makazi ndani ya hifadhi ya mikoko," alisema.
 
"Sisi tulishawauliza wizara wakasema hawajatoa hicho kibali kama Rwakatare anavyodai, sasa kama anacho atuonyeshe.
 
“Hadi sasa hajatuonyesha hicho kibali chake anachodai kinatoa uhalali wa nyumba yake kuwa pale ilipo, yote anayoyasema hayatatuzuia sisi kuibomoa nyumba hiyo.

No comments:

Post a Comment

yes by message

HABARI

Fahamu matukio matano mabaya zaidi viwanjani yaliyoua mamia ya watu

  CHANZO CHA PICHA, GETTY IMAGES Raia wa Indonesia wanataka majibu ya moja ya maafa mabaya zaidi katika historia ya mchezo huo duniani, baad...