Thursday, 7 January 2016

Majaliwa ahitimisha ziara Ruvuma

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, amehitimisha ziara yake ya siku tatu mkoani Ruvuma kwa kuzungumza na waandishi wa habari.
 
Katika majumuisho ya ziara yake aliyoyafanya kwenye ukumbi wa mikutano wa Ikulu Ndogo ya Songea, Majaliwa alielezea kuridhishwa kwake na miradi aliyoikagua.
 
Mbali na kuridhishwa huko, aliwaagiza watendaji wa serikal katika ngazi za halmashauri  kuhakikisha tatizo la madawati kwenye shule za msingi na sekondari, linapatiwa ufumbuzi kwa kutumia vyanzo vya ndani.
 
Aliwataka wakurugenzi wa halmashauri kushirikiana na viongozi wa serikali kuu kutatua tatizo hilo kwa kutumia mbao zinazokamatwa baada ya kuvunwa bila kufuata taratibu, badala ya kuzitunza kwa kuzilundika tu.
 
Kuhusu uchimbaji wa makaa ya mawe unaofanywa katika kijiji cha Ngaka wilayani Mbinga na kampuni ya TANCOAL, Waziri Mkuu alisema serikali inafanya mapitio ya mkataba wa makubaliano kuhusu huduma za jamii.
 
Waziri Mkuu alisema kupitia Wizara ya Nishati na Madini, pia mikataba yote ya kampuni za uchimbaji madini zilizoko nchini ambazo zimeanza kupata masoko ndani na nje ya nchi, itapitiwa upya. 
 
Alisema hivi sasa kuna viwanda vingi vinavyotumia makaa ya mawe, hivyo serikali kupitia wizara yenye dhamana ya madini, itapitia upya mikataba yote ili kuona makubaliano yaliyomo kuhusu huduma za jamii zinazopaswa kutolewa na kampuni hizo. 
 
Kwa mujibu wa Majaliwa, lengo la kufanya hivyo ni kuondoa malalamiko ya muda mrefu, ambayo yamekuwa yakitolewa na wananchi wanaoishi kwenye maeneo yanayozunguka migodi mbalimbali nchini. 

No comments:

Post a Comment

yes by message

HABARI

Fahamu matukio matano mabaya zaidi viwanjani yaliyoua mamia ya watu

  CHANZO CHA PICHA, GETTY IMAGES Raia wa Indonesia wanataka majibu ya moja ya maafa mabaya zaidi katika historia ya mchezo huo duniani, baad...